1 Corinthians 6

Kushtakiana Miongoni Mwa Waumini

1 aKama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2 bJe, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3 cHamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? 4 dKwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa. 5 eNasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio? 6 fBadala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!

7 gHuko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang’anywa? 8 hBadala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.

9 iJe, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 jwala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 kBaadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Isa Al-Masihi na katika Roho wa Mungu wetu.

Dhambi Za Zinaa

12 l“Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote. 13 m“Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili. 14 nNaye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake. 15 oJe, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Al-Masihi mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Al-Masihi na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha! 16 pHamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 17 qLakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.

18 rIkimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. 19 sJe, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 tkwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
Copyright information for SwhKC